KILIMO CHA KAHAWA
Kahawa ni miongoni mwa mazao makuu ya biashara nchini Tanzania. Zao hili hustawishwa zaidi katika nyanda za juu zenye mvua nyingi, hasa Kilimanjaro, Arusha na Kagera. Pia hulimwa kwa kiasi kidogo huko Morogoro, Mbozi, Mbinga, Kigoma na Tarime. Hata hivyo, siku hizi kuna mazao mengine yanayotishia kahawa kwenye medani ya biashara, hasa mboga na matunda. Ili zao hili liweze kuhimili ushindani, sharti wakulima wapanue kilimo chake na waongeze ubora wake.
Ubora wa kahawa unachangiwa na mambo mengi, makubwa zaidi ni: udongo na hali ya hewa stahiki, unyevu tosha, mbegu/miche bora, na ustadi wa mkulima katika kustawisha zao hili. Suala la ustawishaji sahihi wa mibuni liko ndani ya uwezo wa mkulima. Kwa maana hii, mkulima anapaswa kuzingatia kwa makini kanuni zote za kilimo bora cha kahawa, hatua kwa hatua.
Ili kuwa na uhakika wa soko na bei nzuri ya kahawa, inabidi mkulima apande miche yenye sifa nzuri na muonjo unaokidhi matakwa ya wateja. Shamba litunzwe vizuri kwa kuzingatia palizi, kuongeza mbolea, kumwagilia shamba kila inapobidi, na kupogoa au kupunguza matawi. Shughuli zingine muhimu ni kupambana na wadudu au magonjwa yanayoweza kupunguza ukubwa na ubora wa mavuno. Pamoja na kuhakikisha mkulima anachuma matunda yaliyoiva vizuri bila kuyachanganya na mabichi.
Ukiondoa mkoa wa Kagera ambako wakulima wanalima zaidi kahawa aina ya Robusta, karibu sehemu nyingi zilizobaki hustawisha kahawa aina ya Arabica.Tanzania tunazalisha takriban tani 10,000 za aina hii kila mwaka. Makala hii itajikita katika uandaaji wa kahawa aina ya Arabica.
Matunda ya kahawa yanayostahili kuchumwa ni yale yaliyoiva vizuri tu. Yaani yasiwe na rangi ya ubichi au yasiive kupindukia. Hali ya ubichi au kuiva sana kunapunguza ubora wa kahawa, na hivyo kuathiri bei yake kwenye soko. Aidha, ukoboaji wake, yaani uondoaji wa ganda la nje kwa kutumia mashine haukamiliki inavyotakiwa.
Kwanza kabisa, ni muhimu kukoboa au kumenya kahawa mara baada ya kuivuna. Ikobolewe ndani ya saa 8 baada ya kuchumwa. Wakati wa kumenya punje, ni muhimu kutumia maji mengi na safi . Mashine ya kumenyea isafi shwe vizuri mara tu baada ya kazi hiyo. Tenganisha mapepe na maganda ya kahawa ili ubaki na punje safi . Baada ya hapo, kazi inayofuatia ni kuvundika kahawa kwenye kisima kwa lengo la kuondoa utelezi au ulenda. Shughuli hii huchukuwa siku 2 hadi 3. Kisha punje huondolewa na kuoshwa kwa kutumia maji mengi. Osha mara kadhaa. Baada ya hapo, loweka punje hizo kwenye maji safi kwa saa 24. Kisha zioshe mara ya mwisho kuondoa utelezi uliobakia.
Hatua inayofuatia ni ukaushaji. Ubora wa kahawa unaweza kupungua iwapo punje hazikukauka vya kutosha. Kahawa ianikwe mara inapooshwa safari ya mwisho. Ianikwe kwenye chanja maalumu na igeuzwegeuzwe mara kadhaa juani. Ili punje zikauke haraka na kwa usawa, maki au kina cha punje zilizoanikwa kiwe sentimita 2 hadi 2.5. Wakati huohuo, mkulima anapaswa kuchambua punje ili kuondoa
zilizobaki na maganda, au zilizopasuliwa na mashine, au zenye athari ya magonjwa. Iwapo jua ni kali sana, ni vema kusogeza kahawa kwenye kivuli au kuifunika nyakati za mchana, na kuifunuwa kuanzia saa tisa alasiri hadi jioni.
Nyakati za usiku ni muhimu kufunika kahawa kwa kutumia magunia, na kisha kutandika kifuniko cha nailoni ili kuzuia umande na mvua. Kwa kawaida kahawa hukauka baada ya siku 14. Dalili za kukauka kwa punje ni kwamba zikiumwa kwa meno haziwi na ulaini wa kunata, pia rangi ya punje huwa bluu-kijani, bila weusi wowote. Unyevu unaotakiwa kubaki kwenye punje ni kati ya asilimia 10 na 12.
Kahawa iliyokauka vizuri ijazwe kwenye magunia ambayo ni safi. Vizuri kufanya kazi hii asubuhi wakati kahawa imepoa. Kwani ikijazwa mchana wakati ikiwa na joto, kuna uwezekano wa kupata fukuto na hali ya umajimaji. Magunia yaliyojazwa kahawa yawekwe juu ya chaga na yahifadhiwe mahali penye mwanga na hewa ya kutosha. Kwenye hifadhi, usichanganye magunia yenye kahawa na yenye mazao mengine. Aidha, usiyaweke karibu na makasha yenye madawa, kwani kahawa ina tabia ya kuchukuwa harufu ya vitu vingine, hivyo kuharibu muonjo wake wa asili.
No comments