ASALI UZALISHAJI NA UVUNAJI
Asali na nta ni moja ya mazao makuu ya nyuki nchini Tanzania, pia huzalisha nta. Tanzania ina mazingira mazuri ya kuzalisha asali kwa kiwango cha juu cha ubora kutokana na kuwepo kwa aina nyingi ya spishi za mimea inayozalisha chakula
cha nyuki (mbochi na chavua). Kutokana na sababu hizo, asali inaweza kupata soko lenye bei ya juu endapo tutadumisha ubora wake.
Asali hutumika kama chakula, dawa na zao la biashara. Aidha, asali hutumika kama kiambato muhimu katika uokaji, viwanda vya vyakula vitamu, vipodozi, vinywaji na viwanda vya dawa. Kwa mujibu wa Sera ya Taifa ya Ufugaji Nyuki ya Machi 1998 na Programu ya Taifa ya Ufugaji Nyuki ya Novemba 2001, Tanzania huzalisha takriban tani 4,860 za asali. Taarifa ya mwaka 2006 ya Idara ya Misitu na Nyuki inaonesha kuwa Tanzania husafirisha nje ya nchi wastani wa tani 500 za asali. Wanunuzi wakuu wa asali ya Tanzania ni nchi za Ujerumani, Uingereza, Uholanzi, Ubeligiji na Uarabuni.
Licha ya soko zuri la asali, matakwa ya viwango vya ubora vinavyohitajika kwa ajili ya soko la ndani na nje ya nchi hayajawafikia kikamilifu wafugaji nyuki na wadau wengine. Hali hii husababisha kuzalishwa kwa asali yenye kiwango duni na kusababisha zao hili kuuzwa kwa bei ndogo.
ASALI NA MUUNDO WAKE:
Asali huundwa kwa sukari na maji. Kwa wastani asali huwa na sukari kiasi cha asilimia 79.6 na maji asilimia 17.2. Kiasi kikubwa cha sukari zinazounda asali ni fruktosi (asilimia 38.2) na glukosi (asilimia 31.3). Hizi ni aina rahisi za sukari ambazo zinaweza kufyonzwa mwilini kwa wepesi zaidi. Aina nyingine za sukari ni pamoja na malitosi (asilimia 7.3) na sukrosi (asilimia 1.3). Asali pia ina asidi (asilimia 0.57), baadhi ya
protini (asilimia 0.26), kiasi kidogo cha madini (asilimia 0.17) na viasili vya rangi.
UZALISHAJI WA ASALI:
MAANDALIZI YA MIZINGA YA NYUKI
Mizinga itengenezwe kwa malighafi nafuu inayopatikana kirahisi, mbao zilizokauka na ambazo nyuki wanazipenda (pata ushauri kutoka kwa afisa ugani au mfugaji nyuki mzoefu).
Katika maeneo ambayo hayana miti ya kutosha kwa ajili ya kivuli cha kukinga mizinga, vibanda maalum vya nyuki vijengwe ili kuleta kivuli na kulinda makundi ya nyuki Mizinga iambikwe chambo kabla ya kuwekwa kwenye manzuki kwa kutumia nta ya nyuki, gundi ya nyuki au chambo chochote kinachoweza kupatikana katika maeneo husika.
Vianzio vya kujengea masega vitokane na nta nyuki. Mizinga ya nyuki iwekwe kwenye manzuki ambako mfugaji nyuki anaweza kufanya ukaguzi wa makundi ya nyuki pamoja na kuvuna mazao ya nyuki kwa urahisi.
UVUNAJI WA ASALI
Uvunaji wa asali ni vema ufanyike kwa kuzingatia mahali manzuki yalipo. Uvunaji wa mazao ya nyuki kwenye manzuki karibu na makazi ya watu ufanyike wakati wa usiku. Manzuki yaliyoko mbali na makazi ya watu uvunaji ufanyike wakati wowote ili mradi kuna mwanga wa kutosha kumwezesha mvunaji kuona masega kwa urahisi. Tahadhari zichukuliwe ili kuepuka kuchafuliwa kwa asali.
Wafugaji wa nyuki wavune masega yaliyoiva tu. Masega mapya yenye asali iliyoiva yatenganishwe na yale ya zamani ili kupata asali yenye rangi moja. Iwapo kwa bahati mbaya masega yasiyoiva yamekatika, mvunaji anapaswa kuyatenga na kuyatumia kwa ajili ya shughuli zingine, kwa mfano, kula au kuwalishia nyuki.
Matumizi ya viuatilifu hayaruhusiwi wakati wa kuvuna asali. Pia aina yoyote ya kemikali isichanganywe na viwashia bomba la moshi.
Wavunaji wa mazao ya nyuki watumie vifaa maalum vya kinga wakati wa kuvuna. Kiasi kidogo cha moshi baridi kitumike katika kutuliza nyuki.
Vifaa vya kuvunia asali viwe safi, vikavu na vyenye mifuniko isiyopitisha hewa ili kuzuia asali isifyonze unyevu, isiingize uchafu na isichukuliwe na nyuki.
Nyuki lazima waondolewe kwenye masega yanayovunwa.
Masega yenye majana na yenye chavua yasichanganywe na masega yenye asali. Asali iliyochanganywa na majana ni rahisi kuchacha.
Mazao ya nyuki yaliyovunwa yanapaswa kuhifadhiwa mahali penye joto la wastani, pakavu, penye kivuli.
UCHAKATAJI WA ASALI:
Wakati wa uchakataji wa mazao ya nyuki tahadhari na uangalifu wa usafi utiliwe maanani ili kuzuia uchafuzi. Ili kuzuia hali hiyo, wachakataji wa mazao ya nyuki wanapaswa kuzingatia yafuatayo:-
Kutumia vifaa sahihi vya kuchakatia mazao ya nyuki ili kupata mazao bora.
Kuepuka kuchemsha au kupasha moto asali kupita kiasi wakati wa kuchakata. Uchakataji wa asali ya kiwandani, usizidi nyuzi joto
65oC ili kuepuka kuharibu ubora wake.
Kuchuja asali mara baada ya kuvunwa ikiwa bado ina mnato, yaani kabla ya kuanza kuganda.
Kutumia vifaa visivyopata kutu kwa mfano, aluminiamu, enameli, plastiki zinazokubalika, au chuma kilicho galivanishwa ili kuzuia kupata kutu inayoweza kuchanganyika na asali.
FAIDA YA ASALI:
VYAKULA VYA BINADAMU:
Hutumika kama sukari mbadala katika viwanda vya mikate, pia katika mapishi ya aina zingine za vyakula na wagonjwa, pia hutumika kuongeza nguvu kwa wanamichezo na watu wafanyao kazi nzito.
UTENGENEZAJI WA DAWA:
hutumika kama kiambata muhimu cha dawa za kifua, na hutumika kama kitia tamu katika dawa mbalimbali.
– Asali pia inafahamika vyema duniani kote kama mojawapo ya silaha asilia katika kudhibiti magonjwa na matatizo katika mwili. Mfano,
mojawapo ni mchanganyiko wa asali na mdalasini umekuwa ukitumika kutibu maumivu mwilini, kansa, ugonjwa wa moyo, mafua, mashambulizi ya kibofu cha mkojo, kuondoa lehemu mwilini, upungufu wa kuzaa, ugonjwa wa moyo, chunusi, kukatika nywele nakadhalika.
MALISHO YA WANYAMA:
Asali ikichanganywa na malisho inaweza kuongeza hamu ya kula na kuongeza uzalishaji wa maziwa ya ng’ombe, farasi na samaki katika mabwawa ya samaki.
DAWA ZA MIFUGO:
Pia ni mojawapo ya dawa za kutibu ugonjwa wa ng’ombe ujulikanao kama asetomia (acetomia).
VIPODOZI:
Kiambato muhimu katika utengenezaji wa vipodozi mbalimbali na mafuta ya kupaka.
KIFUKUZI:
Hutumika katika utengenezaji wa vifukuzi vya viumbe sumbufu kwa mfano, panya.
UBORA DUNI WA ASALI INAYOZALISHWA:
Hii husababishwa na uelewa mdogo wa mbinu za kuzalisha na mbinu hafifu za uvunaji na kuhifadhi kwenye maghala.
Husababishwa na kutotumia teknolojia za kisasa katika uzalishaji, upotevu hutokea wakati wa uzalishaji, ukosefu wa huduma za ushauri wa kitaalumu kuhusu uzalishaji, na kukosekana kwa mikakati madhubuti ya kuongeza uzalishaji.
Hii hujumuisha ukosefu wa sehemu ya kuuza, usafiri duni toka sehemu za uzalishaji, ukosefu habari za kutosha kuhusu soko, na ukosefu wa nguvu ya pamoja baina ya wazalishaji na kukosekana mikakati madhubuti ya kuongeza uzalishaji.
Pamoja na faida nyingi zilizotajwa hapo juu, tafiti mbalimbali bado zinazoendelea kufanyika. Hivi sasa utafiti unaonesha kwamba uzalishaji wa asali unaweza kuongezwa maradufu kama zao hili litachanganywa na vitu vingine kama vile mdalasini.
Uchunguzi wa kina uliofanywa na gazeti la Habari za Ulimwengu za kila Juma zilichunguza jarida za watafiti wa tiba, wataalamu wa madawa yatokanayo na mimea pamoja na kijarida cha Afya na Lishe na kugundua kwamba kuna umuhimu mkubwa wa matumizi ya asali na mdalasini.
Ugunduzi huu ni muhimu kwa sababu utasaidia kupunguza matumizi ya madawa ambayo hutengenezwa kwa kemikali ambayo ni
hatari kwa afya zetu.
No comments