KILIMO CHA VANILLA
Zao la vanilla ni moja ya zao la viungo ambalo asili yake ni Kusini Mashariki ya Mexico na sehemu nyingine za Amerika ya Kati. Vanilla hulimwa katika nchi mbalimbali duniani. Nchi zinazolima kwa wingi ni pamoja na Madagascar, Comoro, Tahiti, Uganda, India na nchi nyingine za Amerika ya Kati.
Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazolima vanilla katika Afrika. Zao hili lilianza kuingia nchini kutoka Uganda mnamo mwaka 1954 kupitia kwa mkulima mmoja wa kijiji cha Kiilima wilaya ya Bukoba Vijijini. Vanilla imeanza kulimwa kibiashara hasa katika mkoa wa Kagera mwaka wa 1992.
Katika mkoa wa Kagera, kilimo cha Vanilla kimehamasishwa zaidi na Chama cha Maendeleo Ya Wakulima kinachofahamika kama MAYAWA. Chama hiki kimekuwa kikihimiza uzalishaji na usindikaji wa Vanilla ambayo huuzwa kupitia kampuni zilizopo Uganda.
Mmea wa Vanilla huzaa maharage (mapodo) ambayo hukaushwa kwa njia maalum inayowezesha kupatikana kwa Kemikali inayoitwa Vanillini. Kemikali hiyo hutumika katika kuongeza ladha na harufu nzuri kwenye vyakula na vinywaji mbalimbali. Pia hutumika katika viwanda vinvyotengeneza Vipodozi na Dawa za matibabu ya binadamu.
Kwa matumizi ya kawaida, Vanilla huweza kutumika katika vinywaji kama Chai, Maziwa na kama kiungo kwenye mapishi ya Vyakula mbalimbali.
Maeneo mengine ya Tanzania yanayoweza kulima zao la vanilla ni pamoja na wilaya za Mbeya Vijijini, Tukuyu, Morogoro Vijijini, Mvomero, Muheza, Arumeru na Ukerewe.
UMBILE LA MMEA NA MAZINGIRA YANAYOFAA
Mmea wa Vanilla upo katika familia ya Okidi (Orchidaceae) ambayo ina generazipatazo 700. Kati ya hizo, genera moja itwaayo vanilla ndio yenye umuhimu wa kiuchumi. Genera ya Vanilla ina aina au jamii zipatazo 110, kati ya hizo ni mbili ambazo huzalishwa kibiashara. Aina hizo ni Bourbon ya nchini Mexico na Tahitian ya visiwa vya Tahiti.
Mmea wa Vanilla ni rando teke linalotambaa ambalo ni la kudumu. Mmea huu hukua na kutambaa katika mti mwingine hadi kufikia urefu wa mita 10 hadi 15 na zaidi kutegemea na mazingira.
MIZIZI
Mizizi ya mmea huu ni mirefu ina rangi nyeupe, myembamba yenye kipenyo cha milimita mbili. Mizizi hutokea kwenye fundo la shina lililo ndani ya udongo na hutambaa sambamba na tabaka la udongo wenye rutuba. Pia hutokea katika vifundo vya shina sambamba na majani ambayo hujishikiza katika miti ya kuegemea.
SHINA
Shina la vanilla lina rangi ya kijani, refu lenye vifundo na kipenyo cha sentimeta moja hadi mbili. Nafasi kati ya fundo na fundo ni sentimita tano (5) hadi 15.
MAJANI
Majani yana rangi ya kijani iliyokolea, yenye umbile la bapa, lenye ncha, nene na kubwa. Huota kwa kupishana katika shina, yana urefu wa sentimita nane hadi 25 na upana wa sentimita mbili hadi nane, na yana rangi ya kijani iliyokolea.
MAUA
Maua yana rangi mchanganyiko wa kijani na njano na kipenyo cha sentimita 10. Huota katika vifungu vyenye maua kati ya 18 hadi 30.
MATUNDA
Matunda yana umbile la podo la harage lenye rangi ya kijani likiwa changa. Hubadilika kuwa rangi ya njano, hatimaye kahawia kadri linavyokomaa. Podo lina urefu wa sentmeta 10 hadi 25, kipenyo cha sentimeta nane hadi 15 na lina mbegu ndogo sana ambazo huonekana linapokomaa.
MAZINGIRA YANAYOFAA KATIKA UZALISHAJI WA ZAO LA VANILLA
Mmea wa vanilla una asili ya msituni hivyo huhitaji kuoteshwa katika sehemu yenye kivuli na mvua ya kutosha. Ili zao hili liweze kukua vizuri linahitaji mazingira yafuatayo:
MVUA
Mmea wa Vanilla huhitaji kiasi cha mvua cha milimita 1250 hadi 2500 kwa mwaka. Pia zao hili huhitaji kipindi cha miezi mawili cha ukame ili kuweza kusisisimka na kutoa vitumba vya maua.
JOTO
Zao hili hustawi vizuri katika maeneo yenye nyuzi joto 20 hadi 30 za Sentigredi. Pia huweza kustahimili nyuzi joto 32 za Sentigredi. Lakini hukua vizuri zaidi katika kiwango cha nyuzi joto 27 za Sentigredi.
MWINUKO
Zao hili hustawi vizuri katika maeneo yenye mwinuko wa mita 0 hadi 600 kutoka usawa wa bahari. Pia hustawi katika maeneo yenye mwinuko unaofikia mita 1500 katika nchi za joto (tropiki).
UDONGO
Mmea wa vanilla una mizizi ambayo hutambaa katika sehemu ya juu ya udongo. Hivyo, huhitaji udongo mwepesi wa tifutifu, wenye rutuba ya kutosha na usiotuamisha maji.
MWANGA
Mmea wa vanilla huathirika kwa jua na husababisha kuungua kwa majani, hivyo huhitaji kivuli cha asilimia 50 hadi 75 ili uweze kukua vizuri. Kivuli kinaweza kupatikana kwa kupanda miti au kwa kutengenezwa kitaalamu.
UZALISHAJI WA ZAO LA VANILA
Vanilla huzalishwa kwa kupandikiza marando moja kwa moja shambani au kwa kukuzwa kwanza kwenye kitalu na baadaye kupandikizwa shambani. Kabla ya kupanda inatakiwa kuzingatia yafuatayo:
UCHAGUZI WA SHAMBA
Shamba la kupanda vanilla inafaa liwe mahali pasipo na upepo mkali ili kuepuka kuanguka kwa miti ya kuegemea na kukatika kwa mimea. Ni muhimu kupanda miti ya kuzuia upepo ikiwa mahali hapo pana upepo mkali. Shamba hilo pia liwe na udongo usiotuamisha maji, mwepesi na ambao unaruhusu mizizi kupenya kwa urahisi.
Aidha, shamba lisiwe na magugu mabaya (kwa mfano kwekwe/sangare) ambayo hulazimu kutumia jembe mara kwa mara wakati wa palizi. Kutumia jembe huweza kusababisha kukatika au kuharibu mizizi na kuhatarisha ukuaji wa mmea.
UTAYARISHAJI WA SHAMBA
Utayarishaji wa shamba huhusisha shughuli mbalimbali kama vile usafishaji wa shamba, utayarishaji wa mashimo na uwekaji wa mbolea.
KUSAFISHA SHAMBA
Shamba lisafishwe kwa kulima, kungíoa visiki, magugu mabaya na kutifua hadi kina kisichopungua sentimita 30.
KUTAYARISHA MASHIMO
Mashimo yatayarishwe miezi miwili hadi mitatu sambamba na usafishaji wa shamba. Yawe na kina cha sentimita 30 na upana wa sentimita 60 hadi 90. Nafasi kati ya mstari na mstari iwe mita mbili na nusu hadi mita tatu na kati ya shimo na shimo iwe mita moja na nusu hadi mbili. Udongo wa juu utengwe na ule wa chini.
UWEKAJI WA MBOLEA
Mbolea za asili kama mboji, vunde au samadi ichanganywe vema na udongo wa juu na kujazwa kwenye shimo kwa kipimo cha debe moja hadi mbili kwa kila shimo.
MIFUMO YA UPANDAJI
Zao la vanilla huweza kupandwa shambani kwa kutumia mifumo mikuu mitatu ifuatayo:
(i) VANILLA PEKEE
Mfumo huu unahusisha upandaji wa mmea wa vanilla na miti ya kuegemea tu ambayo hutoa kivuli kwa mimea.
(ii) VANILLA NA MIGOMBA
Mfumo huu unawezesha kuotesha vanilla katika shamba la migomba, ambapo rando hupandwa pamoja na mti wa kuegemea ndani ya shamba la migomba. Na hivyo kukuwezesha kufanya kilimo cha migomba na vanilla katika shamba moja kwa wakati mmoja
(iii) VANILLA NA MITI YA KIVULI
Katika mfumo huu vanilla huoteshwa katika shamba la miti ya kivuli, ambapo mmea hupandwa na miti ya kuegemea katikati ya miti ya kivuli.
Kumbuka: Mfumo wa pili na wa tatu unapendekezwa zaidi kutokana na matokeo yake mazuri.
UPANDAJI WA MITI YA KUEGEMEA (MIEGA)
Miti ya kuegemea hupandwa miezi miwili hadi mitatu kabla ya kupanda rando la vanilla ili iweze kuchipua, kutoa kivuli na kuwa na uwezo wa kuhimili mimea.
(i) SIFA ZA MIEGA
Miti inayofaa kutumika kwa kuegemea iwe na sifa zifuatazo:
- Uwezo wa kukua haraka bila kuathiri mmea wa vanilla.
- Uwezo wa kutoa kivuli kinachofaa.
- Uwezo wa kuchipua haraka inapopunguzwa.
- Uwezo wa kuchipua matawi kwa chini ili kupandishia marando kwa urahisi.
- Uwezekano wa kuoteshwa kwa urahisi.
Miti yenye sifa hizo ni pamoja na mibono (Jatropha carcus) na Gilirisidia. Miti mingine inayoweza kutumika kwa kivuli na kuegemea ni pamoja na Erythrina spp na Bauhania spp.
(ii) KUPANDA MIEGA YA MIBONO
Miti inayotumika zaidi katika mashamba ya vanilla ni jamii ya Jatropha. Miti hii huoteshwa kwa kutumia mbegu au kipande cha tawi kwa umbali wa sentimita 30 kutoka katika shimo la kupandia vanilla. Tawi la mbono lenye urefu wa sentimita 120 hadi 150 hupandwa katika kina cha sentimita10 hadi 15.
UPANDAJI WA VANILLA
Mmea wa vanilla hupandwa mwanzoni mwa msimu wa mvua ili kuhakikisha upatikanaji wa unyevu ardhini. Hupandwa kwa kutumia rando lenye urefu wa kati ya sentimita 100 hadi 150 (futi tatu na nusu hadi tano) kutoka kwenye mmea unaokuwa vizuri, usio na magonjwa na wenye pingili ndefu. Rando lenye sifa hizo hukua haraka na kutoa maua mapema (miaka 2). Rando fupi halikui haraka na huchukua muda mrefu kutoa maua (miaka 2 hadi 3).
KUTAYARISHA MARANDO
- Kata rando kwa kutumia kisu kikali kwa kufuata vipimo (sentimita 100 hadi 150).
- Ondoa majani matatu hadi matano katika sehemu ya chini ya rando itayofukiwa kwenye udongo.
- Ning’iniza rando lililokatwa kwenye kivuli kwa muda wa siku saba hadi 10 kabla ya kupanda ili kupunguza utomvu na kulipa nguvu ya kuchipua na kuhimili hali ya shambani.
JINSI YA KUPANDA
Upandaji wa vanilla hufanywa kwa kutumia hatua zifuatazo:
- Andaa nyasi kavu (matandazo) ambazo zitatumika mara baada ya kupanda.
- Tengeneza kifereji chenye kina cha sentimita 10 hadi 12 katikati ya shimo lenye mbolea lililokwisha tengenezwa.
- Laza sehemu ya rando iliyotolewa majani katika kifereji hicho, acha sehemu yenye majani juu ya ardhi.
- Fukia rando kwenye kifereji kwa udongo na gandamiza taratibu ili lishikamane na udongo.
- Funga sehemu ya juu ya rando kwa kutumia kamba katika umbile la nane kwenye mti wa kuegemea.
- Weka matandazo kuzunguka kila shina lililopandwa.
KUMBUKA:
- Utaratibu huu wa kupanda hutumika katika aina zote za mifumo ya kuzalisha vanilla, na hutofautiana kwa nafasi za upandaji kati ya mfumo mmoja na mwingine.
- Shamba la vanilla pekee katika miaka ya mwanzoni, huweza kuchanganywa katikati ya mistari na mazao mengine ya muda mfupi kama mazao ya jamii ya mikunde.
UTUNZAJI WA SHAMBA
Vanilla huhitaji kutunzwa vizuri ili iweze kukua vizuri na kutoa mavuno yenye ubora wa hali ya juu. Huduma muhimu katika uzalishaji wa vanilla ni kama ifuatavyo:
KUTENGENEZA KIVULI
Mmea wa vanilla huhitaji kivuli ili uweze kukua vizuri. Hivyo ni muhimu kupanda miti ya kivuli kabla ya kustawisha vanilla. Katika ukuaji wake kuanzia inapopandwa hadi inapokaribia kutoa maua huhitaji kivuli cha kutosha kinachoweza kuzuia jua kali na kuruhusu mwanga (asilimia 60 hadi 70).
Kipindi cha kusisimua kivuli kipunguzwe zaidi na kufikia asilimia 55 hadi 50. Kivuli kitengenezwe kwa kupunguza matawi ya miti ya miega na ya kivuli ili kupata kivuli kinachofaa.
Kumbuka: Kivuli kizito huathiri ukuaji wa mmea.
KUWEKA MATANDAZO
Utandazaji wa nyasi ni muhimu katika shamba la vanila kutokana na tabia ya ukuaji wa mizizi ambayo huota katika kina cha sentimita 5 hadi 10, hivyo huhitaji kulindwa isiharibiwe. Matandazo yawekwe kuzunguka mashina ya mimea ili kuhifadhi unyevu, kuzuia uotaji wa magugu, na kulinda mizizi isiharibiwe wakati wa palizi.
Kumbuka: Matandazo yawe makavu na yasiwe na mbegu za magugu.
PALIZI
Palizi hufanyika wakati wowote magugu yanapoota shambani. Inashauriwa kufanya palizi kabla ya mvua kunyesha ili mmea uweze kutumia maji ya mvua ipasavyo. Palizi ifanyike wakati wowote magugu yanapoota shambani, kwa kungíoa magugu kutumia mikono ili kuepuka kujeruhi mizizi jembe linapotumika.
KUNING’INIZA MARANDO
Mmea wa vanilla uliokua vizuri huota matawi (marando) mengi na marefu. Marando hayo huelekezwa kwenye matawi ya miti ya kuegemea na kuningíinizwa. Rando linapofikia urefu wa sentimita 150 hadi 180 liningíinizwe katika matawi ya miega ili liendelee kukua kuelekea chini. Endapo kuna upepo mkali, marando yafungwe kwenye miega kwa muda ili yasivunjike.
KULISHA MARANDO
Kulisha marando ni kitendo cha kufukia ardhini sehemu ya kipande cha rando ili kiweze kutoa mizizi na kuongeza nguvu ya kuchukua chakula kutoka kwenye udongo. Kazi hii hufanywa baada ya rando lililoningíinizwa kurefuka sana kiasi cha kutambaa ardhini, katika hatua hii mmea huweza kuwa na umri wa miezi sita hadi tisa kutegemea na utunzaji.
Jinsi ya Kulisha
- Ondoa majani matatu hadi manne kwenye rando lililoingíinizwa na kurefuka sana.
- Fukia kwenye udongo, karibu na shina sehemu iliyoondolewa majani.
- Weka matandazo katika sehemu iliyofukiwa ili kuhifadhi unyevu.
- Funga sehemu ya juu ya rando katika mti wa kuegemea ili liendelee kukua.
- Marando mawili hadi mitatu yalishwe kwa wakati mmoja na mengine yaachwe kwa ajili ya kutoa maua na kupata marando ya kupanda.
Kumbuka: Kulisha kufanyike wakati wa mvua ili marando yaweze kutoa mizizi kwa urahisi. Kazi hii irudiwe kila wakati ili rando mama litakapokatika machipukizi yake yaendelea kukua.
KUSISIMUA
Kusisimua ni kitendo cha kuufanya mmea kuwa katika hali ya kuweza kutoa maua. Kitendo hiki kifanywe wakati mmea ukiwa umefikia umri wa mwaka 1 na nusu au zaidi, na hufanywa wakati wa kiangazi ili kuepuka kupata matawi mengi badala ya vitumba vya maua. Mmea usiosisimuliwa hautoi maua au hutoa maua machache na kusisimua mapema kunaweza kuuchosha mmea.
JINSI YA KUSISIMUA
- Chagua matawi matatu hadi matano yanayoningíinia. Kusisimua matawi mengi kunaweza kuudhoofisha mmea au kuzaa maharage madogo.
- Kata ncha ya rando ili kuwezesha vitumba vya maua kukua na kuwa tayari kufunguka au kutoa maua.
Ukataji wa ncha huweza kufanyika kama ifuatavyo:
- Kukata ncha ndogo (mdomo wa rando) kwa mkono. Hii hufanyika kwa rando fupi linaloningínia.
- Kukata rando kwa kisu kikali, kwa rando linaloningínia ambalo halijafikia urefu wa kupanda.
- Kukata rando kwa kisu kikali kwa rando refu linaloningíinia (lenye urefu wa kuweza kupandwa, sentimita100-150).
UCHAVUSHAJI
Ni kitendo cha kuunganisha chavua kutoka katika sehemu dume ya ua na kuweka katika sehemu jike ya ua, hufanyika baada ya maua kuchanua.
UCHANUAJI WA MAUA
Mmea wa Vanilla hutoa maua miezi miwili hadi mitatu baada ya kusisimuliwa. Maua huchanua kwa kipindi cha masaa matatu hadi manne kuanzia saa tatu asubuhi hadi saa saba mchana kwa muda wa miezi miwili hadi mitatu kutegemea unyevu uliopo kwenye udongo na kiwango cha Jua.
Ua huchanua kwa muda huo na hudondoka baada ya siku 1 ikiwa halikupata chavua. Hivyo ni muhimu uchavushaji ufanyike kwa haraka na kwa uangalifu mkubwa.
JINSI YA KUCHAVUSHA
Mmea wa vanilla, ili uweze kutoa matunda inabidi uchavushwe. Ua la vanilla kwa kawaida huchavushwa na nyuki jamii ya melapona ambao hawapo hapa nchini. Nyuki hao hupatikana Mexico na katika nchi nyingine za Amerika ya Kati. Hivyo uchavushaji hufanywa kwa mikono kwani umbile la ua haliruhusu nyuki wa aina nyingine kufanya uchavushaji.
UCHAVUSHAJI HUFANYWA KWA KUFUATA HATUA ZIFUATAZO:
- Gawa petali ya ua la vanilla katika sehemu mbili kwa kutumia pini, sindano, au mwiba. Hakikisha vifaa hivyo ni safi.
- Kunjua sehemu jike ya ua (stigima) kwa kuelekea juu ili kuwezesha kulala sambamba kwenye sehemu dume ya ua (stameni).
- Unganisha stameni na stigima na kubana taratibu kwa dole gumba kwa nusu dakika ili kuruhusu chavua kuingia kwenye stigima.
Ua lililochavushwa vizuri, hubaki likiningíinia kwenye kikonyo chake. Ikiwa uchavushaji haukufanikiwa, ua hudondoka baada ya siku moja au mbili. Kiasi cha maua au mapodo nane hadi 12 yaachwe katika kila kitumba. Aidha vitumba vinne hadi nane viruhusiwe kukua katika kila rando na visizidi 20 kwa mmea.
No comments