KILIMO CHA NYANYA CHUNGU
KILIMO CHA NYANYA CHUNGU
KILIMO CHA NYANYA CHUNGU : Zao hili pia hujulikana kwa jina la “Nyanya Chungu”, “Ngogwe” au “Ntongo”. Huu ni mmea wa kitropiki, na kustawi kwake karibu ni sawa na bilinganya.
Mmea hukua na kufikia urefu wa mita moja hadi moja na unusu na matawi na majani yake hufanya kichaka.
Nyanya mshumaa zinaweza kuwekwa katika makundi mawili: yaani aina itoayo matunda madogo madogo na machungu sana na aina itoayo matunda makubwa na machungu kidogo.
Rangi ya matunda huwa kijani kibichi au kijani-njano, au njano-nyeupe, na yakipevuka kabisa hugeuka mekundu.
Matunda yafikia hatua ya kupevuka huwa hayafai tena kuliwa, ila kwa kutoa mbegu za kupanda. Matunda hupikwa au kukaangwa na kufanywa mchuzi, au huchanganywa na mboga zingine. Pia hupikwa pamoja na ndizi.
KUPANDA: Miche huoteshwa kwa kupanda mbegu ambayo husiwa kwenye kitalu na kutunzwa kama mazao mengine.
Miche ifikiapo kimo cha sentimeta 10 hadi 15 hupandikizwa bustanini, kwa umbali wa sentimeta 90 kwa 90, hadi 120 kwa 120; hii kutegemeana na ukubwa wa kichaka chake.
Mimea ya “Ngogwe” hutunzwa kama bilinganya, huhitaji ardhi yenye rutuba na unyevu wa kutosha. Mazao huanza kuvunwa miezi miwili baada ya kupandikizwa, na uvunaji huendelea kwa muda mrefu kidogo.
MAADUI: Nyanya Mshumaa ni mmea mgumu, kwani unaweza kustahimili upungufu wa maji kuliko aina nyingine za Mboga.
Vile vile haushambuliwi sana na baadhi ya Magonjwa yasababishwayo na mvua au uchepechepe mkubwa. Ingawa yako magonjwa na wadudu ambao hushambulia zao hili, madhara yake si makubwa sana kiasi cha kutisha au kumkatisha tamaa mkulima. Usafi wa bustani na kubadilisha mpando wa mazao, vinaweza kuondoa tishio hilo.
KUVUNA: Mboga huvunwa wakati zikiwa bado mbichi. Ili ziweze kukaa kwa muda mrefu (hata majuma mawili) bila kuharibika, inapendekezwa kuzichuma pamoja na sehemu ya vikonyo vyake. Vikonyo hivyo hukobolewa wakati wa kuzitayarisha kupikwa. Kwa hiyo, zao hili linaweza kusafirishwa hadi masoko ya mbali bila kuharibika.
No comments